MEA CULPA MEA
CULPA MEA MAXIMA CULPA
(NIMEKOSA MIMI NIMEKOSA MIMI NIMEKOSA SANA)
Basi katika nchi za ulaya hadithi nyingi zilitapakaa, Makala
nyingi zikachapwa na waandishi mahiri waliobobea katika fani hiyo, wote
wakijaribu kusema kile wanachokijua kuhusu Nchi yenye mashimo tu, na mashimo
hayo yanauwezo wa kuongea.
Mwalimu Jones Fernandes katika kitabu chake cha WONDERS OF
THE TALKING HOLE, alijaribu kuelezea kile anachokijua kuhusu nchi iliyojaa
mashimo yenye uwezo wa kunena,alisema pengine ni mabaki ya miili ya watu wa
kale yamejumuika na kutengeneza uhai wa kiumbe kisicho onekana kiishicho ndani
ya mashimo hayo.
Mchunguzi wa maswala ya miamba kutoka uingereza bwana Peter
schzech naye alikaliliwa akisema pengine ni miamba iliyoko chini ya ardhi
imekuwa ikisuguana na hivyo basi kupelekea sauti ikasikika kutoka katika mashimo
yale ambayo hayajulikani yalichimbwa na nani na kwa kusudi gani kwani ni ya
muda mrefu sana.
Swala hili lilichukuliwa kwa uzito na wanafunzi kutoka chuo
kikuu cha OXFORD Ambao waliamua kwenda kufanya uchunguzi juuu ya nchi ya
mashimo yanayoongea, walipofika kule walishangazwa sana, nchi zima yalijaa
mashimo tu wasingeweza kutembea kilomita moja bila ya kukutana na shimo kubwa
sana, na kilichowashitua zaidi ni kwamba kulikuwa na sauti zilizosikika kutoka
katika mashimo yale zikisema “MEA CULPA MEA CULPA MEA MAXIMA CULPA”maneno ya
kilatini yenye maana sawa na “NIMEKOSA MIMI NIMEKOSA MIMI NIMEKOSA SANA” Hakika
walishangazwa na sehemu ile, kwani hakukuwa na Binadamu wa aina yoyote ile.
Basi watafiti wale walikaza moyo na kujitosa kuingia katika
mashimo yale ikiwa ni moja ya mbinu ili waweze kutambua chanzo cha sauti ile,ili
wagarimu masaa kadhaa mpaka kufika ndani kabisa ya mashimo yale, kule
walishangaa walichokiona, waliwaona wazee na vikongwe wakisujudu mbele ya
vijana na watoto wadogo huku wakisema kwapamoja MEA CULPA MEA CULPA MEA MAXIMA
CULPA(NIMEKOSA MIMI NIMEKOSA MIMI NIMEKOSA SANA), wazungu wale walishangazwa na
jamii ile kwani walikuwa ni watu masikini sana, hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa
amevalia nguo isiyo na tundu, wote walionekana kuwa wachafu. Vijana walikuwa
wameshikilia fimbo za mikwaju huku wakiwacharaza wazee wale ambao walikuwa
wakiendelea kusujudu mbele yao wakisema nimekosa mimi nimekosa mimi nimekosa
sana.
Wazungu wale walijaribu kuwauliza vijana wale na watoto wale
ni kwanini wanawacharaza vile babu na bibi zao,wale vijana waliwaangalia
wazungu wale kwa jaziba nyingi huku wakionyesha kuwa sio watu wema sana
kwao.kijana mmoja kati ya wale alitoka mbele na kuanza kusema huku akilia
sana………….
“Ni bora mmekuja ninyi, maana napo wangekuja babazenu bado
tungewaunganisha na kuwaadhibu kwa pamoja bila ya kujali wadhifa wao, hawamnao
waona ni mabepari wanchi hii myaka kadhaa iliyopita, ni baba na babu zetu.
Tumekuwa tukiwauliza ni kwanini tunaishi kwenye mashimo kwa muda mrefu lakini
wamekuwa hawana majibu kamili. Tumewauliza uko wapi udongo waliotoa kwenye
mashimo haya ili tuurudishie japo nasisi tupate raha ya kuishi kwenye tambalale
kama ilivyokuwa wao hapo zamani, lakini cha kushangaz hata udongo hawajui ni
wapi waliuweka. Tumepata mafunzo kadhaa kutoka hukoo dunia yenye tambalale kuwa
hapo mwanzo nchi hii ilikuwa tambalale, na ilipendeza kwa kila aliyeitizama. Watu
kutoka magharibi walikuja kutazama maajabu ya Nchi hii, hawa Babu zetu hawa,
wakatumia mema ya Nchi hii ili kujinufaisha wao, tumepata taarifa kuwa
kulikuwako na mawe yenye thamani kubwa kiasi kwamba jiwe moja lingeweza
kusomesha watoto wengi kuanzia chekechea mpaka Elimu ya juu. Nayo tumeuliza
hawajui tena yalipo, na cha kushangaza zaidi hatujui mawe yale yaliyochimbwa
yameleta faida gani katika kaya zetu” aliongea kijana mmoja huku akiwaacha
midomo wazi wageni wale kutoka mataifa ya nje ambao walikuja kufuatilia
chimbuko la sauti kutoka kwenye mashimo iliyokuwa ikisikika inasema MEA CULPA
MEA CULPA MEA MAXIMA CULPA.
Basi kwa ghafla wazungu wale walijikuta tayari wamezungukwa
na kundi lile la watu huku wakiwatembezea kichapo cha hatari, wazungu wale waliomba
radhi kwa watu wale walioonekana kuwa ni wenye hasira kali, basi na wao kwa
uchungu walianza kuimba maneno waliyokuwa wakiyatamka wazee wale “MEA CULPA MEA
CULPA MEA MAXIMA CULPA”. Kwa huzuni sana alisimama mzee mmoja kati ya wale
waliokuwa wakiadhibiwa na kusema…………
“vijana wapendwa naomba mnisikilize, ni kweli tumekosa na
tumekosa sana, kiasi cha kushinda masaa 24 tukisujudu mbele yenu huku tukiimba
MEA CULPA MEA CULPA MEA MAXIMA CULPA, yaani NIMEKOSA MIMI NIMEKOSA MIMI
NIMEKOSA SANA,ila hao wageni mngewaacha ila nao wakaongee na babu zao
wawajulishe kuwa kile walichotushauri kimesababisha leo hatuishi kwa Amani”
alisema Mzee Yule na kuendelea kusujudu pamoja na wenzake.
Hakika maneno ya Mzee Yule yalionekana kuwa ni ya busara
sana, wageni wale waliamriwa kuondoka ili wakawapashe habari babu na bibi zao
walichokikuta kule. Wageni wale waliondoka huku wakiwa wanamaumivu makali sana,
wote walienda kuwaonyesha wake zao Alama za mijeredi wake zao huku wakiendeleza
kusambaza ukweli juu ya Nchi yenye Mashimo yanayoongea.
Na L.A.MUGISHA.
Comments
Post a Comment